Shughuli za Uinjilishaji wa kina zinazotekelezwa na Shirika la Roho Mtakatifu nchini Tanzania
Shirika la Roho Mtakatifu linapojiandaa kuadhimisha mkutano mkuu wa Shirika kwa mara ya kwanza Barani Afrika huko Bagamoyo, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican imeendelea kukujuvya kuhusu vigezo vilivyopelekea hadi Tanzania ikachaguliwa kuwa ni mwenyeji wa mkutano huu wa kihistoria kwa Shirika na Kanisa la Tanzania kwa ujumla. Hii ni kutona na umaarufu wa Mji wa Bagamoyo kuwa ni chimbuko la Kanisa Katoliki Afrika Mashariki. Padre Philip Massawe amefafanua kwa kina fukuto la Uinjilishaji wa kina Visiwani Zanzibar na baadaye Tanganyika na Kenya.
Leo, Mheshimiwa Padre Massawe anatumegea kwa undani zaidi kuhusu shughuli za Uinjilishaji wa kina zinazofanywa na Shirika la Roho Mtakatifu katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili. Wamejikita katika Uinjilishaji awali, huduma za kichungaji Parokiani.
Shirika la Roho Mtakatifu limekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma katika sekta ya afya, elimu pamoja na kukuza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo Visiwani Zanzibar ili kujenga msingi wa uelewano, upendo na mshikamano, kila mtu akijitahidi kuheshimu imani ya jirani yake na wote kwa pamoja wakipania kutafuta mafao ya wengi na maendeleo ya Jamii wanamoishi.