Social:

RSS:

Vatican Radio

The voice of the Pope and the Church in dialogue with the World

language:
Vatican Radio

Home / Family

Familia ni shule ya maisha ya Kikristo, tunu za kibinadamu na kitovu cha ushuhuda wa imani, matumaini, mapendo, ukarimu na upatanisho!


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2012, wakiyaangalia matukio makuu kwa mwaka huu, hususan Kongamano la Saba la Familia Kimataifa pamoja na mambo mengine wanachambua kwa kina na mapana kuhusu Familia.
Maaskofu wanasema, familia ni shule ya maisha ya Kikristo, tunu za kibinadamu na kitovu cha ushuhuda wa imani, mapendo na ukarimu na upatanisho. Kutukumbusha zaidi ndani ya viunga vya Radio Vatican ni Sr. Gisela Upendo Msuya. RealAudioMP3
Familia ya Kikristo ni mahali muafaka sana pa kuishi maisha ya ushuhuda, ni Kanisa la nyumbani, ni jumuiya inayoamini na inayoinjilisha, jumuiya iliyo katika mazungumzano ya kudumu na Mungu na iliyo tayari na wazi kumtumikia Mungu na jirani kwa ukarimu.
Aidha, ni katika familia ambapo wazazi wanapaswa kuishi maisha ya kishuhuda kwa kupendana, kuaminiana, kuheshimiana, kubadilishana mawazo, tunu na mielekeo, kushirikishana hali ya furaha na uchungu, mafanikio na majaribu, kuliko katika jumuiya yoyote ile.
Ni katika familia ambapo wazazi, kwa maneno, matendo na mifano yao, wanapaswa kuwa watangazaji wa kwanza wa Injili kwa watoto wao. Kama vile Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unavyofundisha, familia ni “Kanisa la nyumban” lenye wajibu wa kurithisha imani ya mababu, kudumisha mapokeo ya kiimani na kupeleka sala za pamoja kwa Mungu na kutafsiri katika maisha ya kila siku misimamo yake ya kiimani.
Familia ni mahali ambapo baba wa familia, mama, watoto na wanafamilia wote wanatelekeza ukuhani wao walioupata kwa njia ya ubatizo, na kwa namna ya pekee kwa njia ya kupokea Sakramenti, sala na shukrani, ushuhuda wa maisha ya utakatifu na kujitoa kwa upendo hai. Kwa hiyo, familia ni shule ya kwanza ya maisha ya Kikristo, shule ya tunu za kibinadamu. Ili familia iweze kuwa kitovu cha ushuhuda wa maisha ya Kikristo, wazazi wana wajibu wa kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata mafundisho ya msingi ya imani ya Kikristo kwa usahihi na kina.
Kwa bahati mbaya, eneo hili lina changamoto nyingi, kwa sababu wazazi wengi hawajachukulia kwa makini wajibu wao wa kuwa watangazaji na warithishaji wa kwanza wa imani kwa watoto wao. Katika familia nyingi, kuna ushahidi wa kutosha uonaoonyesha kwamba watoto hawapati nafasi ya kusikia mara kwa mara mambo yanayohusu imani yao kutoka katika vinywa vya wazazi wao.
Wazazi wengi, licha ya kutumia gharama nyingi kuwatafutia watoto wao elimu ya kidunia, suala la kuhakikisha watoto wao wanapata elimu na malezi ya dini halitiliwi mkazo sana. Tunashuhudia katika siku zetu hizi wazazi wakihangaika mno kutafuta shule ambazo zitawasaidia watoto wao waijue kwa ufasaha elimu dunia, lakini hawafanyi hivyo kuhusu elimu ya dini.
Matokeo yake, watoto wanakuwa na ufahamu mkubwa wa elimu dunia na ya viumbe mbali mbali, lakini wanakuwa na ombwe kubwa la elimu juu ya Yeye aliyeumba vitu vyote! Elimu ya dini imeachwa kuwa jukumu pekee la shule zinazomilikiwa na Kanisa au la walimu wa dini. Na mara nyingi mambo yanayohusu imani hayapati nafasi katika maongezi na katika shughuli za kila siku za kifamilia.
Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunapotafakari agizo na amri ya Bwana “Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu”, ni vyema wazazi mkajikumbusha wajibu wenu wenye heshima ambao unawadai kuwa watangazaji wa kwanza wa Injiili na wa tunu za maisha ya Kikristo kwa watoto wenu.
3.2.4.2. Wahudumu wa Daraja Takatifu
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika Tamko juu ya Huduma na Maisha ya Mapadri, unatufundisha kwamba, Wahudumu wa Daraja Takatifu wanapaswa kuishi maisha ya ushuhuda kwa kuchuchumia maisha ya ukamilifu. Tangu kuwekwa wakfu katika ubatizo wao, vile vile kama waamini wote walipokea ishara ya kipaji cha wito, na Neema ambayo ni kubwa sana, kiasi kwamba, hata katika hali ya udhaifu wa kibinadamu, wana uwezo na wana wajibu wa kutafuta ukamilifu kadiri ya fundisho la Bwana: “Basi nanyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa Mbinguni alivyo mkamilifu” (Mt 5:48).
Mtaguso unasisitiza kwamba Mapadri hasa inawapasa kuelekea ukamilifu huo, kwa sababu wao, kwa kujaliwa kupokea kwa mara nyingine, uwakfu kwa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, wanateuliwa na kuwekwa katika hali ya kuwa vyombo vilivyo hai vya Kristo aliye Kuhani wa milele, ili waendeleze kazi yake ya ajabu.
Mtaguso unaongeza kwamba, Mapadri, wakitimiza huduma ya Roho na ya haki, wanatayarishwa katika maisha ya kiroho, ikiwa lakini, watachukua wajibu kwa mafundisho ya Roho wa Kristo anayewapa uhai na kuwaongoza. Kwa sababu ni kwa njia ya matendo matakatifu wanayotimiza kila siku, kama vile kwa njia ya huduma yao nzima, wanayotimiza kwa kushirikiana na Askofu na wao kwa wao, kwamba wanapata mwelekeo bora kwa ajili ya ukamilifu wa maisha yao.
Lakini, “ni utakatifu wenyewe wa mapadri, kwa upande wake, unaosaidia kwa vikubwa kutimiliza kwa mafanikio huduma yao” na kwa kweli, hali ya utakatifu katika parokia na katika jimbo, kwa kiasi kikubwa inategemea utakatifu wa maisha ya mapadri. Kwa sababu, ingawa Neema ya Mungu ina uwezo wa kutimiza kazi ya wokovu hata kwa njia ya wahudumu wasiostahili, (taz PO 12) hata hivyo Mungu kwa kawaida anapenda kudhihirisha matendo yake makuu kwa kutumia wale ambao, wakijifanya watiifu mbele ya msukumo wa uongozi wa Roho Mtakatifu, wanaweza kusema pamoja na Mtume, kutokana na umoja walio nao na Kristo na utakatifu wa maisha: “Ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu” (Gal 2:20).
Hivyo basi, kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima, kwa namna ya pekee, ni mwaliko pia kwa Wahudumu wa Daraja Takatifu kujipima kwa makini ili kuona kama Neno la Mungu wanalolisoma na kulihubiri kila siku wanalishika ndani yao wenyewe. Yawapasa kuzingatia fundisho la Mtume Paulo kwa Timoteo: “uyatafakari hayo, ukae katika hayo, ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafanikio yako. Dumu katika mambo hayo, maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikilizao pia” (1Tim 4:15-16), ili liwe mwongozo kwao, hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, iwapo wanataka kutekeleza agizo la Bwana “Enendeni Mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu” (Mt 28:19).
3.2.4.3